Daktari Jela Miaka Minne kwa Kuua Akimtoa Mimba Mwanafunzi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miaka minne jela, Daktari Nicholaus Matomola, baada ya kukiri kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Jubilate Shao, wakati akimtoa ujauzito.

Mahakama hiyo ilipewa kibali cha kusikiliza kesi ya mauaji ya bila kukusudia ili kupunguza mrundikano wa mahabusu, lengo likiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jitihada za kumaliza kesi zilizoko mahakamani kwa muda mrefu.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Msajili wa Mahakama Kuu, Mustapha Siyani, baada ya mshtakiwa kukiri kosa hilo.

Hakimu Siyani alisema kwa kuwa mshitakiwa amekiri kwamba alifanya mauaji ya bila kukusudia, mahakama inamhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka minne.
“Mahakama hii imekutia hatiani kwa kosa hilo na inakuhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mine,” alisema Hakimu Siyani.

Kabla ya hukumu hiyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali, Florida Wencelaus na Agatha Lumato, ulimsomea mshitakiwa mashtaka yake yaliyoonyesha kuwa Februari 19, 2010 akiwa katika zahanati ya B.T Diognostic Centre iliyoko karibu na hosteli za Mabibo, Shao (wakati wa uhai wake) alikwenda kupata huduma ya matibabu.

Ilidaiwa kuwa Shao alikwenda kwenye zahanati hiyo kwa lengo la kutoa mimba lakini kwa bahati mbaya mauti yalimfika kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

Wencelaus alidai kuwa baada ya uchunguzi wa daktari kufanyika, Shao alibainika kuwa na majeraha katika viungo vya uzazi yaliyomsababishia kifo chake.

Mshtakiwa alipewa muda wa kujitetea ili apunguziwe adhabu na ndipo alipodai kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba tayari amekaa mahabusu kwa miaka sita. Aliongeza kwamba ana mke na watoto watatu wanaomtegemea, hivyo kuomba apunguziwe adhabu.

Alidai kuwa ni kweli alimuua Shao bila kukusudia wakati akimtoa ujauzito katika zahanati yake.
Powered by Blogger.