Mwanafunzi wa UDOM auawa kwa kupigwa na wenzake wakati wakitoka baa

Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Fredrick Joseph (25), ameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo na watu wanaosadikiwa kuwa ni wanafunzi wenzake wakati akitoka klabu ya pombe (Bar).

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la chuo hicho ambapo mwanafunzi huyo alisikika akipiga kelele ndipo walinzi wakafika na kumkuta akiwa anagalagala njiani.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, amesema mwanafunzi huyo ambaye ametokea Musoma mkoani Mara alishambuliwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiofahamika.

Amebainisha mwanafunzi huyo alikutwa majira ya saa 10 alfajiri katika eneo hilo la chuo hicho huku akisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu huyo alikuwa na ugomvi na watu hao katika klabu ya pombe ya Canival Pub iliyopo chuoni hapo.

“Alipoondoka kurudi bwenini akiwa njiani alishambuliwa na watu hao wasiofahamika na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, kipigo kilichosababisha kifo chake wakati alipokimbizwa kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma,” alisema Mambosasa

Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi na hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Alipoulizwa kuwa taarifa za mwanafunzi huyo kushambuliwa na wenzake, Mambosasa alisema kwasababu inadaiwa haifahamiki upelelezi bado unaendelea.

“Kwa sababu mwenye bar si yupo, kama kuna ugomvi ambao ulikuwa unaendelea tutajua tu, nimemuelekeza OCD kufuatilia ni nani waliokuwa wanakunywa kwenye hiyo bar chuoni, ni lazima tu watakuwa wanachuo ili tuwabaini,”

Kamanda huyo amesema ameelekeza uchunguzi wa kina ufanyike kama kulikuwa na ugomvi ndio hao hao walienda kumtegea njiani.

Chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutaja jina lake kwa madai kuwa  siyo msemaji wa polisi kimesema kuwa marehemu Joseph alikuwa anakunywa pombe pamoja na marafiki zake lakini baada ya kulewa walianza ugomvi ambao hata hivyo waliamuliwa.

“Baada ya kuamuliwa ule ugomvi wa awali ndipo wenzake walipokwenda kumsubiria kwa mbele kwenye kichaka ambapo walimvamia na kumshambulia na kumwacha karibu ya kufa,” kilisema chanzo hicho.

Kiliongeza kuwa, baada ya kumwacha hapo na kutoweka ndipo walinzi wa chuo hicho waliokuwa doria walimuokota na kumfikisha kwenye kituo kidogo cha polisi kilichopo Chimwaga ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alipofariki wakati akipatiwa matibabu.

Chanzo hicho kimesema hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayeshikiliwa na polisi kwa kuwa wote waliomshambulia walitoroka na hawajulikani walipo.
Powered by Blogger.