Wachezaji wa Azam FC- wawafariji watoto yatima Chamazi......

WACHEZAJI wa klabu ya Azam FC mchana wa leo wametembelea kituo cha kulelea watoto yatima, kijulikanacho kama Yatima Group Trust Fund, kilichopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mabingwa hao wapya wa Bara walifika katika kituo hicho baada ya sala ya Ijumaa wakiongozwa na Mkuu wa msafara, Katibu wa timu, Nassor Idrissa Mohammed ‘Father’ na kukabidhi misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na jezi, seti ya king’amuzi cha Azam TV na dishi lake, na vyakula na vinywaji.
Pamoja na hayo, wachezaji wa Azam FC walionyesha upendo kwa watoto hao kwa kujumuika nao na kufurahi pamoja. Watoto hao walijibu kwa kushangilia ‘Azam Azam’. 
Nahodha wa Azam FC, John Bocco kulia akiwa na Msaidizi wake, Salum Abubakar 'Sure Boy' wakikabidhi seti ya king'amuzi cha Azam TV kwa viongozi wa Yatima Group kushoto leo mchana.

Mmoja wa Maofisa wa kituo hicho, akitoa hutuba yake kwa msafara wa Azam, inayomilikiwa na kampuni ya Bakhresa Group Limited, alishukuru kwa ujio huo na akasema kituo hicho ni mashabiki wakubwa wa Azam na siku zote wamekuwa wakiunga mkono timu hiyo na sasa wanafurahia mafanikio yake.
Alisema kampuni ya Bakhresa Group inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa kituo hicho.
Alisema Bakhresa amekuwa akilisha chakula wakati wote katika kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1996 na kupata usajili wake Machi 3, 2001 kabla ya kupewa leseni ya makazi mwaka 2002, wakati jiwe lake la Msingi liliwekwa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi mwaka 2004.
Aliwataja wafadhili wengine wa kituo hicho kilichoanza na watoto 45 ambao sasa wameongezeka hadi kufika 173 kuwa ni Rais Mstaafu Mwinyi, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hary Kitilya na Naibu Waziri wa zamani wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Shamim Khan.
Alisema kituo hicho chenye wafanyakazi 15, kipo chini ya uongozi wa Mwenyekiti Winfrida Lubanza, Mweka Hazina Haruna Mtandika, Freddy George Katibu na DK James Lace, ambae ni raia wa Marekani.
Alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo fedha za ada za shule kwa watoto wanaowasomesha, majengo ya kituo kutokuwa ndani ya uzio jambo ambalo si salama kwa watoto na mishahara ya wafanyakazi wake.
Akaomba wadau wajitokeze kusaidia zaidi ili kuwezesha kupunguza gharama za uendeshaji na Meneja wa Azam FC, Jemadari Said akizungumza baada ya hotuba hiyo, alisema; “Tumeyasikia mliyoyazungumza, tunashukuru tutayafanyia kazi,”.

Katika watoto 173 wanaolelewa kwenye kituo hicho, watoto 40 wanasoma Vyuo Vikuu mbalimbali ndani na nje ya nchi, 60 wapo katika shule za sekondari, 53 shule za Msingi, 15 Chekecheka na 15 wengine hawajafikia umri wa kwenda shule.
Azam ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Jumapili, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, huku waliokuwa wapinzani wao katika mbio za taji hilo, Yanga SC wakishinda 2-1 dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha.
Azam imefikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho kesho, kwani Yanga SC yenye pointi 55 sasa ikiifunga Simba SC itafikisha 58.
Licha ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wake Aprili 13, mwaka huu, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo
Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.
Powered by Blogger.