Sh. Bilioni 1/= za Wanafunzi Hewa Zarudishwa

Tangu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kutaka vyuo 29 vilivyokuwa na wanafunzi hewa kurudisha Sh. bilioni 3.85 kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Sh. bilioni moja zimerudishwa tayari.

Kiasi hicho kinafanya fedha zilizorudishwa bodi ya mikopo tangu ukaguzi wa wanafunzi hewa kuanza kufikia Sh. bilioni 3.6.

Sh. bilioni 2.6 zilirudishwa HESLB siku chache tu baada ya Prof. Ndalichako kutangaza kuanza uhakiki wa wanafunzi hewa ambao wanalipwa mikopo, mwezi uliopita.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru alisema wamefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha kutoka kwenye baadhi ya vyuo ambavyo vilitakiwa kufanya hivyo.

Alisema baadhi ya vyuo havijawasilisha fedha hizo na badala yake vimewasilisha ufafanuzi ni kwa nini ukaguzi wa awali ulionyesha kwamba vina wanafunzi hewa.

“Baadhi ya sababu wanazoziainisha ni kwamba wakati wa uhakiki wanafunzi ambao hawakukutwa wengine walikuwa wanaumwa, wengine walikuwa wamesafiri na wengine wanasema wanafunzi hao walikuwa mwaka wa mwisho kwa hiyo wameenda nyumbani,” Badru alisema.

Alisema mara baada ya kupokea ufafanuzi wa vyuo hivyo, bodi itapima kisha kukabidhi kwenye timu iliyoundwa na Waziri Ndalichako.

Alisema kwa vyuo ambavyo havitarejesha fedha hizo kama vilivyotakiwa, vitakatwa kwenye zile ambazo kila muhula hupelekwa.

“Wale ambao hawatarejesha fedha tutawakata kwenye mgawo wa fedha za mikopo ambazo hupelekwa kila muhula,” alisema.

Akizungumzia kuhusu mwitikio wa urejeshaji wa mikopo kwa hiari kwa wanufaika, Badru alisema baada ya tangazo la majina ya wadaiwa sugu wa kwanza kuchapishwa kwenye magazeti, zaidi ya watu 2,000 wamejitokeza kurejesha.

“Wapo wanaorejesha wenyewe na wengine kupitia waajiri wao, lakini mwitikio ni mkubwa kwa sasa wanaorejesha fedha hizi,” alisema.

Awali Prof. Ndalichako alilieleza gazeti hili kwamba vyuo vilivyorudisha fedha kabla ya ukaguzi ni Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambacho kiliongoza kwa kurudisha kiasi kikubwa, ambacho ni zaidi ya Sh. milioni 400.

Wakati wa ukaguzi Udom ilibainika kuwa na wanafunzi hewa 364 ambao kwa mwaka wa fedha uliopita walilipwa jumla ya Sh. milioni 460.96.

Katika orodha ya vyuo 31 vilivyokaguliwa, chuo cha Mtakatifu Agustino (Saut-Mbeya) na Chuo Kikuu cha Biashara (CBE-Dodoma) havikuwa na wanafunzi hewa.

Chuo ambacho kilikutwa na majina hewa mengi zaidi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambacho kati ya wanafunzi 13,972 wanaopata mikopo, 350 walibainika kuwa ni hewa wakiwa wamelipwa Sh. milioni 703.43.

Akifafanua juu ya fedha zilizorudishwa mara baada ya kutoka kwa tangazo la uhakiki wa wanafunzi, Prof. Ndalichako alisema sheria inataka fedha zikikaa siku 30 chuoni bila kuchukuliwa, zirudishwe bodi.

“Lakini hilo lilikuwa halifanyiki, ila tulivyosema tunakagua, fedha hizo zilirudishwa ndani ya muda mfupi.”
Powered by Blogger.