Marais EAC Kukutana kwa Dharura Jijini Dar es Salaam Chini ya Mwenyeji Wao Rais Magufuli

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika Jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitisha Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Septemba, 2016.

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na Mawaziri vilivyofanyika Jijini Arusha utajadili agenda kuu nne ambazo ni:- Mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA).
Agenda zingine ni Kupokea Taarifa ya Mwezeshaji wa mazungumzo ya Amani nchini Burundi, Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania; Kupata taarifa ya hatua za kukamilisha uanachama wa Sudan Kusini kwenye EAC; na Kuapishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Rwanda.

Akizungumzia mkutano huo kwa Waandishi wa Habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa mkutano huu umeitishwa kwa dharura ili kuzungumzia agenda hizo muhimu hususan ile ya nchi wanachama kukubaliana kwa pamoja kusaini au kutosaini Mkataba wa EPA ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016.

Kuhusu Mkataba wa EPA, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya ya kushirikiana kibiashara kupitia EPA miaka 14 iliyopita na kuingia makubaliano ya awali mwaka 2014.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano hayo ya awali EU na EAC zilikubaliana Mkataba huo usainiwe kwa pamoja na nchi zote za Jumuiya mwezi Julai 2016 kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Hata hivyo Tanzania ilitangaza kutosaini makubaliano hayo kwa sababu mkataba huo unaweza kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania nchi ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo 2025.

Aidha, Tanzania inahitaji kujadiliana zaidi na nchi wanachama ili kujiridhisha kuwa mkataba huo hautoathiri Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan hatua ya mwanzo ya mkataba ambayo ni Umoja wa Forodha.

Kuhusu nchi nyingine wanachama Mhe. Mahiga alieleza kwamba, tayari Kenya na Rwanda zimesaini mkataba huo huku Uganda ikisubiri majadiliano ya nchi wanachama kabla ya kusaini na Burundi ikijitoa kusaini mkataba huo kwa vile tayari nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo vya kiuchumi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07 Septemba 2016.
Powered by Blogger.