Waziri Mkuu Apokea Hundi ya Sh. Mil. 50 Kutoka NSSF

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa sh. milioni 50 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kusaidia ujenzi wa shule ya sekondari Lindi iliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.

NSSF imetoa msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake iliyoitoa  Julai 17, 2016 katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya hiyo iliyoendeshwa na Waziri Mkuu .

Katika ajali hiyo, shule ya sekondari Lindi iliathirika kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia yaliungua na kusababishia hasara ya sh. milioni 682.78.
Akipokea msaada huo leo (Jumanne, Agosti 30, 2016) Waziri Mkuu ameushukuru uongozi wa shirika hilo na kuwaomba wadau wengine waliotoa ahadi wazitekeleze ili waweze kukamilizsha ujenzi wa majengo hayo.

“Naamini fedha hizi zitakwenda kufanya kazi ambayo NSSF wameikusudia. Na leo hii naikabidhi kwa Meya wa Manispaa ya Lindi pamoja na  Mkurugenzi wake ili waende kuzifanyia kazi,” amesema.

Baada ya kukabidhiwa hundi hiyo na Waziri Mkuu, Meya wa Manispaa ya Lindi, Mohamed Lihumbo amelishukuru shirika hilo kwa kutimiza ahadi waliyoitoa siku ya harambee na kwamba fedha hizo hazitapotea kwa sababu zinaenda kutumika katika malengo yaliyokusudiwa.

Meya huyo amesema baada ya kukamilisha ujenzi wa shule hiyo wataanda hafla na kuwaita wadau wote waliotoa michango yao kwa ajili ya ujenzi huo ili wakaone matumizi ya michango waliyoitoa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius Kahyarara amesema msaada huo ni sehemu ya mpango wa shirika hilo wa kusaidia jamii katika mambo mbalimbali kwa mujibu wa sera iliyowekwa na shirika hilo.

“NSSF imekuwa kinara kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutoa misaada mbalimbali ya kijamii ambapo imejiwekea sera ya kusaidia katika sekta za elimu, afya na huduma nyingine muhimu za kijamii,” amesema.

Prof. Kahyarara amesema misaada hiyo haiathiri michango ya wanachama wa mfuko huo na mafao yatolewayo kwani hutokana na faida inayopatikana kwa uwekezaji makini wa mfuko huo.

Habari na Ofisi ya Waziri Mkuu
Powered by Blogger.