Rais Magufuli Kufungua Maadhimisho ya Wahandisi

Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), Eng. Steven Mlote akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu maadhimisho ya 14 ya Siku ya Wahandisi Tanzania itakayoadhimishwa Septemba mosi jijini Dar es Salaam.(Picha Zote Na Benjamin Sawe – Maelezo).

****

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya kumi na nne ya Siku ya Wahandisi yatakayofanyika Septemba mosi hadi pili jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo ya siku mbili yanatarajiwa kukutanisha zaidi ya wahandisi elfu mbili kutoka ndani na nje ya nchi ili kupata fursa ya kufanya majadiliano ya kitaaluma, kufanya maonesho ya kiufundi na kibiashara, kuwatambua na kuwazawadia wahandisi wahitimu waliofanya vizuri katika mafunzo yao ya mwisho na kuwaapisha wahandisi waliokidhi vigezo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), Eng. Steven Mlote amesema mada kuu katika maadhimisho hayo itakuwa ni “TANZANIA KUELEKEA KUWA NCHI YA UCHUMI WA KATI NA KUWA NCHI YA VIWANDA: NINI JUKUMU LA WAHANDISI”.

“Tumejipanga Siku ya Wahandisi mwaka huu iwe na mvuto wa pekee kwa sababu mada yake ni ya kitaifa ikiangalia Dira ya Maendeleo ya Taifa na mwelekeo wa nchi kuwa nchi ya viwanda” amesema Eng. Mlote.

Maadhimisho ya wahandisi Tanzania yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 2013, lengo likiwa ni kuiwezesha jumuiya ya wahandisi nchini kuionesha jamii kile ambacho wahandisi wanaweza kukifanya katika kuleta maendeleo ya nchi.

Takribani wahandisi elfu 17 wanakadiriwa kuwepo nchini katika sekta mbalimbali, lengo likiwa ni kuwa na wahandisi elfu 83 ili kukidhi mahitaji ya nchi kuwa ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Powered by Blogger.