Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake waendelea kusota Rumande

Uamuzi wa ombi la kufutiwa mashitaka ya utakatishaji wa fedha lililowasilishwa na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake, unatarajiwa kutolewa Aprili 27 mwaka huu.

Uamuzi huo ulitakiwa kutolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Emillius Mchauru, aliahirisha kwa sababu hajamaliza kuuandika.

Hakimu Mchauru alisema, alipewa majukumu mengine ya kikazi, akashindwa kuandika uamuzi huo, lakini imebaki sehemu ndogo hivyo atausoma Jumatano ya Aprili 27, mwaka huu.

Mbali na Kitilya, wengine katika kesi hiyo ni mrembo wa zamani wa Tanzania ambaye pia alikuwa Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa benki hiyo, Sioi Graham Solomon.

Washitakiwa wote wapo rumande kwa kuwa kisheria mashitaka ya utakatishaji wa fedha ambayo wanaomba yafutwe hayana dhamana.

Katika ombi lao walilowasilisha kupitia jopo la mawakili likiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa, waliiomba Mahakama iwafutie mashitaka hayo kwa kuwa hati ya mashitaka haina maelezo yanayokidhi vigezo vya kisheria vya mashitaka hayo.

Mgongolwa alidai ili mashitaka yawe ya utakatishaji wa fedha, ni lazima kuwe na hatua nne; kwanza kuwe na kuwekwa kwa fedha, kuhamishwa kwa fedha na fedha kuwekwa kwenye shughuli za kiuchumi kwa lengo la kuficha, pia kuwe na chanzo kichafu cha fedha.
Powered by Blogger.