Nani Mkali leo Kati ya Diamond na Mzee Yusufu???/

HATIMAYE imewadia! Kama ulikuwa ukijiuliza ni sehemu gani ya kutoka Sikukuu ya Krismasi ya leo basi ni ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem, jijini Dar ambapo kampuni ya simu ya Vodacom kwa kushirikiana na kampuni ya vinywaji ya Cocacola na Red Bull watawashusha wakali ambao hawashikiki Bongo kutoa burudani mwanzo mwisho.
WAKALI WA SARAKASI NDANI
Ukumbi utafunguliwa leo mapema kuanzia asubuhi ambapo moto wa burudani utaanza rasmi huku kundi linalotikisa kwenye sarakasi na mazingaombwe, Masai Worriors likiwapa burudani ya aina yake watoto.
Masai watawaonyesha watoto maajabu mbalimbali sambamba na kuwachezesha michezo kibao kama vile kucheza kwenye magunia, kugombania kiti, kucheza na moto na kuwaonyesha staili kibao za sarakasi.

BINGWA WA BAISKELI ‘TETE’ ATAKUWEPO
Mbali na Masai Worriors pia bingwa wa kucheza na baiskeli, John Mwaipaya ‘Tete’ atakuwepo kuwapagawisha watoto kwa kujikunjakunja kwa kila staili huku akitumia baiskeli.

Kuhakikisha burudani kwa watoto haikauki, watapata kuburudika pia na michezo kama kubembea, kuteleza, kuogelea na mashindano ya kuimba, kula ice cream, kupaka rangi za uso na kuvaa vinyago spesho usoni huku kila mtoto atakayefika ukumbini hapo atahakikisha anarudi na rundo la zawadi nyumbani kwao.

USIKU WA WAFALME KUACHA HISTORIA
Kuanzia usiku wa saa moja, shoo ya kibabe itaanza ambapo pazia la burudani litafunguliwa kwa wasanii wanaong’ara kwenye muziki wa Bongo Fleva kama vile Pamela Daffa ‘Pam D’, kundi linalotikisa na ngoma yao ya Umebadilika kwa sasa huku likifananishwa na kundi mahiri kutoka Kenya, Sauti Sol linalotambulika kama Kazi Kwanza Band, Kawina na wengine wengi watapanda jukwaani na kukamua nyimbo zao zinazobamba kitaani.
MZEE YUSUF, JAHAZI KUFUNGA MWAKA
Burudani itaanza kunoga zaidi pale atakapopanda mfalme wa muziki wa Taarab, Mzee Yusuf akiwa sambamba na kundi lake la Jahazi Modern Taarab, ambapo usiku wa leo atahakikisha anafunga mwaka kwa staili ya aina yake ukumbini hapo kwa kupiga nyimbo zao zote zinazobamba kutoka katika albamu zao mbalimbali.

Miongoni mwa nyimbo watakazozipiga ni kutoka katika albamu ya Wasiwasi Wako, Mpenzi Chocolate, My Valentine, Daktari wa Mapenzi, Wagombanao na Tupendane Wabaya Waulizane.

Jahazi pia watahakikisha wanawaonjesha mashabiki ngoma zao kali zilizopo katika albamu yao mpya na ya sita inayobamba ya Chozi la Mama kama vile Alipangalo Jalali, Tiba ya Mapenzi, Aso Kasoro ni Mungu, Fanya Yako na nyingine kibao.Mashabiki wategemee kuusikia wimbo mpya kutoka Jahazi ambao ni habari ya mjini kwa sasa, Mahaba Niue.

DIAMOND KUANDIKA HISTORIA MPYA
Ikumbukwe kuwa mara ya mwisho Diamond Platnumz kutinga ukumbini hapo ilikuwa ni katika uzinduzi wa Video ya Muziki Gani akiwa na Nay wa Mitego uliofanyika Mei mwaka jana. Usiku huo uliacha historia kubwa kutokana na mashabiki kufurika ukumbini hapo.

Katika usiku wa leo uliopewa jina la Usiku wa Wafalme, ambapo mkali wa Afro Pop, Diamond atahakikisha anaweka historia mpya ambayo haitasahulika kwa shabiki yeyote atakayefika ukumbini hapo.

Kuonyesha shukrani kwa mashabiki wake kwa kumpa sapoti, atatinga ukumbini na tuzo zake zote tatu alizozinyakuwa mwishoni mwa mwezi uliopita kutoka Channel O Africa Music Video Awards (CHOAMVA).
Sapraiz kubwa atakayoitoa ni pamoja na kufanya shoo kwa kutumia vyombo vya muziki ‘live band’ kwa mara ya kwanza huku akiwatambulisha madensa wake wapya.

Usiku huo Diamond atahakikisha anapiga nyimbo zake kali zaidi ya 20 bila kupumzika na burudani itakolea zaidi pale atakapokamua nyimbo kama Mdogomdogo, My Number One na hii ambayo ni habari nyingine kwa sasa, Nitampata Wapi.
Powered by Blogger.