DKT SLAA; UZEMBE WA WANACHADEMA NDIO USHINDI WA CCM

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza mikutano yake ya nchi nzima kama ilivyotangazwa na katibu mkuu wa chama hicho Dkt Wilbroad Slaa, hivi karibuni alipozungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.

Chadema kimeridhia kufanya mikutano nchi nzima ambapo katika mkoa wa Iringa mkutano huo ulianza jana katika viwanja vya Mlandege kwa kuhutubiwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu mwenyekiti wa CHADEMA Prof Abdalla Safari.
Akizungumza na mamia ya watu waliojitokeza katika mkutano huo ambao imeelezwa kuwa haujawahi kutokea mkutano kuwa na wimbi la watu kama hao, amesema kuwa ukombozi wa nchi ya Tanzania umetokana na damu ya watanzania hivyo hakukuwa na sababu ya watanzania kuishi maisha ya umasikini kama ilivyo kwa nchi kama hii yenye rasilimali nyingi ikiwa ni pamoja na misitu, madini na ardhi ya kutosha.


Safari alisema kuwa wananchi wa Botswana wanafaidika na madini ya nchi yao kwa serikali kukusanya 70% ya madini huku nchi kama Tanzania ikichukua 5% ya madini, hivyo ni dhahiri kuwa Uwezo duni wa kufikiri kwa viongozi wa Tanzania ndio sababu ya umasikini wa Watanzania na utajiri wa wananchi wachache (Mafisadi).

"Pia nawaahidi kwamba UKAWA tumeridhia kusimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi kuanzia ngazi ya serikali za mtaa hadi Taifa, lakini kubwa zaidi tunataraji kwenda mahakamani kuzuia mchakato wa katiba kukusanya maoni ya wananchi" Alisema Safari

Hata hivyo Katibu mkuu wa CHADEMA Taifa, Dkt Wilbroad Slaa amesema kuwa kuna daftari la mkazi linapita mtaani hivyo wananchi wanapaswa kujiandikisha kwa wingi ili wawe na uwezo wa kupiga kura sambamba na kujitokeza kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa.

"Mnapaswa kutambua kuwa siku 21 kabla ya kupiga kura ni muda wa kujiandikisha hivyo kila mmoja ajiandikishe na kuhamasisha wengine, nachukua nafasi hii kuwakumbusha kuwa uzembe wa wanachadema ndio ushindi wa CCM" Alisema Slaa.

Slaa alisema kuwa CCM imeshindwa kutoa elimu bure kwa watanzania kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu tangu waingie madarakani hivyo wasitegemee kufanikiwa kwa kipindi kifupi kilichosalia.

Naye mbunge wa Jimbo la Iringa mjini Mch Peter Msigwa alijibu mapigo ya Katibu mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana alipozuru Mkoani Iringa hivi karibuni, alisema katibu huyo alitumia muda mwingi katika mkutano wake kumzungumzia badala ya kuzungumzia maendeleo ya nchi.

"Nilishinda kwa ushindi mnono mwaka 2010 kwenye uchaguzi mkuu hivyo nawaomba msikubali kupotoshwa na propaganda ya kwamba nilishinda baada ya CCM kujichanganya, tuna mambo mengi ya kuzungumza lakini tutaendelea kuonana mara kwa mara kwani muda wetu hautoshi, wapo waliosema mimi na Chiku Abwao tuna ugomvi hivyo ni rahisi kukomboa Jimbo la Iringa Mjini, hilo lisahaulike naamini mmemsikia wenyewe Chiku alichokisema"

Msigwa alisema kuwa kuhusu mfuko wa jimbo ameanza kupita kila Kata ili kutoa ufafanuzi kwa kina kwa kile kilichofanyika hatimaye watanzania kutopotoshwa na baadhi ya wanasiasa.

Kwa upande wake Salumu Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu mkuu wa Chadema Zanzibar amesema kuwa, Chadema kinaamini katika vijana ndio maana wengi wao ni viongozi na ufanisi wa hoja unaonekana.

Mwalimu alitumia nafasi hiyo pia kumuomba ruhusa Katibu mkuu wa chama hicho ili kurejea tena mkoani Iringa kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa lengo ikiwa ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha na kujitokeza katika kuwania nafasi za serikali za mtaa.

Viongozi wengine waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Patrick Ole Sosopi Makamu Mwenyekiti BAVICHA Taifa sambamba na Chiku Abwao Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa.
Powered by Blogger.