AMKA! Vishawishi vya kimapenzi kwa wanafunzina namna ya kuviepuka
Naendelea kuelezea jinsi wanafunzi wanavyoweza kushinda vishawishi vya kuingia kwenye mapenzi.
Ni wajibu wa mwanafunzi kugomea zawadi inayokuja kwa mlango wa nyuma, kwa vile watafiti wanasema watu tisa kati ya kumi wanaosaidia husaidia ili wajisaidie ni mmoja tu anayesaidia kwa maana ya kusaidia.
Ni wajibu wa mwanafunzi kugomea zawadi inayokuja kwa mlango wa nyuma, kwa vile watafiti wanasema watu tisa kati ya kumi wanaosaidia husaidia ili wajisaidie ni mmoja tu anayesaidia kwa maana ya kusaidia.
MAZINGIRA MAGUMU –Mazingira magumu yametajwa sana na baadhi ya wanafuzi kuwa yanashawishi kufanya mapenzi, lakini ukweli unabaki kuwa mwanadamu kamili mwenye kujitambua hawezi kuuza utu wake kwa kukwepa adha. Mwanafunzi hana budi kupambana na shida za kitambo ili atafute raha ya muda mrefu.
Kujilegeza kokote kwa lengo la kujiokoa na mateso hakujawahi kuwa na matokeo mazuri kwa mtu au taifa lolote duniani zaidi ya maangamizi. Mwanafunzi lazima afahamu kuwa kukubali kuwa mtumwa wa mapenzi ya mtu hakutamuokoa bali kutamfelisha masomo na kisha kutelekezwa na pengine kuambulia magonjwa ya zinaa ukiwemo UKIMWI.
Ili kuweza kushindana na mazingira magumu ni vema mwanafunzi akafikiria faida za kusoma na kufaulu na hasara za kufanya mapenzi na hivyo kuweka akilini sababu za kuvumilia shida hizo kwa muda kwa faida ya muda mrefu kwenye maisha.
MABADILIKO YA MWILI-Ni jambo linaloshawishi, kwani mwili unapofikia wakati wa kubalehe huleta usumbufu kwa watoto na kuwafanya wawe na tamaa ya kufanya mapenzi. Lakini tamaa hizi ni rahisi mno kuzishinda, tofauti na zile zitakazokuja baada ya mtu kuanza mapenzi. Njia pekee ya kuzishinda ni kuepuka vishawishi vyote na kuwa na maamuzi sahihi kama tunavyoendelea kujifunza.
KULAGHAIWA –Laghai kubwa kabisa ambayo inachukua nafasi ya kwanza kwa sasa ni ya ahadi za uchumba. Wasichana wengi wamejikuta wakiingia katika uhusiano wa kimapenzi na wanaume waliowachukulia kama wachumba wao. Ukweli ni kwamba matapeli wengi wa kimapenzi hutumia mwanya huu kuwadanganya wanafunzi na kuwaharibia masomo yao. Kama wewe ni mwanafunzi, usikubali kabisa mtu akuite mchumba na akiwa na sababu ya kufanya hivyo mwelekeze kwa wazazi wako lakini wewe usizungumze naye kwa kuwa umri wako bado mdogo.
MALEZI YASIYO NA MAADILI-Wazazi nao wanaweza kuchangia mwanafunzi kujiingiza katika mapenzi, kuna baadhi yao hudiriki kuwatumia watoto wao kama mitaji kwa kuwauza kwa wanaume kwa lengo la kujipatia mahitaji yao. Lakini wengine hushawishi kwa matendo yao, yaani kufanya matendo ya kihuni mbele za watoto na hivyo kuwafanya waone kama mapenzi si kitu cha hatari kwa vile baba na mama wanafanya.
Ushauri kwa mwanafunzi ni kuwa makini na kukataa kila vishawishi hata kama vinatoka kwa wazazi wao. Inaaminika kwamba kila mwanadamu ana haki ya kusimamia anachokiamini hasa kinapokuwa cha kweli, la sivyo kuacha maadili kwa sababu ya mtu mwingine hakuna tofauti na kuuza utu.
Lakini njia nyingine nzuri kwa mwanafunzi kujitambua kuhusu upotoshaji wa wazazi kitabia ni kuangalia malezi na mafanikio ya watoto wengine ambao wanaheshimika katika jamii na kuiga tabia zao ikiwa pamoja na kuwaomba ushauri walimu na watu wenye busara sehemu anayoishi.
KUKOSA MIPAKA- Kuna wanafunzi ambao hawaheshimu mipaka ya uhusiano kati ya wanaume na wanawake. Utakuta chumba cha wavulana, wasichana wanaingia kwa uhuru hadi usiku wa manane na wakati mwingine kuwa tayari kushikanashikana hadi sehemu nyeti za miili yao.Tabia hii haipendezi kwani inaweza kuleta hisia za kimapezi.
Inashauriwa kuwa wanafunzi wa jinsia tofauti lazima wawe na mipaka ya uhusiano kwa kuheshimiana. Haifai wanafunzi wa jinsia mbili tofauti kukumbatiana hovyo na inapotokea wakawa pamoja basi wazingatie sababu za msingi za umoja wao na si vinginevyo.