Mbowe, polisi uso kwa uso makao makuu

Jopo la Wanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), pamoja na wanachama wake, wanatarajia kuunganisha nguvu leo kumsindikiza Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, kuelekea Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya mahojiano na maofisa wa jeshi hilo.

Jeshi hilo limemuita Mbowe, lakini chama chake kinasema hakielewi kiongozi huyo anaitwa kwa sababu zipi.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Willibroad Slaa, alisema Mbowe atakwenda polisi leo kwa lengo la kuitika wito wa jeshi hilo.Dk. Slaa, alisema uamuzi wa Mbowe kuitikia wito wa kwenda kuhojiwa na jeshi hilo
ulitokana na Kamati Kuu iliyokaa juzi licha ya kwamba barua ya wito huo haielezi sababu za kuitwa kwake.Naibu Katibu Mkuu Bara ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema wameweka nguvu kubwa ya wanasheria watakaomsindikiza mwenyekiti wao wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.Aliwataja wengine ambao wamethibitisha kuungana na Lissu kuwa ni Mabere Marando ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatara na wanasheria wengine wa chama hicho ambao hawakutajwa majina.Alisema mbali na wanasheria wa chama, lakini pia wanasheria wengine wanaweza kuongezeka kwa kuwa wametoa wito kwa wanasheria wengine watakaopata nafasi ya kuungana na hao.Akizungumzia suala hilo, Lissu alisema yeye kama Mwanasheria Mkuu wa chama hakukubaliana na wito wa jeshi hilo kwa kuwa barua haikuwa inaeleza sababu za Mbowe kuitwa na kuhojiwa, lakini baada ya Kamati Kuu kukaa waliamua aende.

“Barua ya Jeshi la polisi ilitakiwa kueleza sababu ya wito, ushauri wangu kama mwanasheria nilikuwa nimesema asiende, lakini kwa sababu tulijua jeshi letu halifuati sheria na mara nyingi hutumia nguvu, Kamati Kuu ikashauri kwamba aende,” alisema Lissu.

Aidha, Dk. Slaa, alisema kuwa wanaamini kwamba wito wa kuitwa Mbowe umetokana na shinikizo la Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro alilotamka wazi bungeni Jumatatu wiki hii usiku na kusema atahakikisha maandamano yaliyotangazwa na Chadema ya kupinga Bunge Maalum la Katiba hayafanyiki.

Alisema msimamo wa kufanya maandamano bado upo pale pale na kwamba tayari baadhi ya vikundi katika ngazi mbalimbali vimeanza kuwasilisha ripoti ya maandalizi ya maandamano hayo na pindi yakikamilika wataeleza kwa vyombo vya habari siku rasmi ya kuanza.

Dk. Slaa alisema maandamano yaliyotangazwa na Chadema ni ya amani ambayo Jeshi la Polisi halikutakiwa kuyazuia isipokuwa lingetakiwa kufahamu yanaanza lini ili kuimarisha ulinzi kama sheria inavyoeleza.

Alisema chama chochote cha siasa chenye usajili kina haki ya kufanya maandamano bila kuzuiliwa na mtu yeyote.

KAULI YA POLISI
Wakati chama hicho kikimruhusu Mbowe kwenda kuhojiwa, Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa mpango wa kumhoji kiongozi huyo upo palepale.
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Hezron Gimbi, alisema jana siku ya Mbowe kuhojiwa anayeijua ni Issay Mngulu, ambaye amekuwa akiwasiliana na kiongozi huyo.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya kumtaka Rais kusimamisha Bunge Maalum la Katiba, Dk. Slaa, alisema maamuzi hayo hayakuwa ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pekee kama baadhi ya wajumbe wa kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wanavyozungumza katika vyombo vya habari, bali yalikuwa ni maamuzi ya vyama vyote vilivyoshirikishwa na TCD kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, Dk. Slaa, alisema kati ya mambo ambayo Kamati Kuu iliazimia katika kikao chake cha juzi ni pamoja na kushirikiana na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya CUF na NCCR-Mageuzi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Desemba mwaka huu ili kuhakikisha wanashinda viti pamoja na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Suala lingine ni kuendelea na msimamo wa kufanya maandamano nchi nzima wa kuwashawishi wananchi wasipige kura ya kuikubali Katiba mpya, ikiwa Bunge hilo litaendelea kung`ang`ania na uchakachuaji wa Rasimu ya katiba hiyo.

Akifafanua kuhusiana na madai kwamba wajumbe wa Ukawa walitoka katika Bunge la Katiba wakiwa wamesaini fedha za vikao, Lissu alikanusha na kusema kwamba mwisho wao kusaini fedha ilikuwa Aprili 14 na Aprili 16 walitoka bungeni.

MAANDAMANO DODOMA YAFUTWA
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limezuia maandamano ya Chadema kwa maelezo kuwa yanapinga Bunge Maalum la Katiba ambalo lipo kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula, alisema wamepokea taarifa kutoka kwa chama hicho kikitaka kufanya maandamano kuanzia viwanja vya Mwalimu Nyerere hadi bungeni.

Alisema pia taarifa hiyo imeeleza kusudio la kufanya maandamano ya amani katika wilaya zote za mkoa huo leo kupinga mchakato wa Bunge hilo unaoendelea mjini hapa.

“Jeshi la Polisi linalinda sheria zilizopo na mtu anayepinga Bunge la Katiba kwa sasa ni uvunjifu wa sheria kama anataka aende mahakamani,pia nawaomba wananchi msiende kushiriki katika maandamano kwani ni batili na yanafanyika siku ya kazi,” alisema Lukula.

Alisema alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Chadema kwa zaidi ya saa mbili, lakini hawakubaliana kutokana na viongozi hao kusisitiza kuandamana leo.
 
crdt: NIPASHE
Powered by Blogger.