Binamu yangu amenibaka

Mkazi mmoja wa kijiji cha Mloe, mkoani Kilimanjaro aliyejulikana kwa jina moja la Agustin (47) anadaiwa kumbaka na kumpa mimba binamu yake mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa) aliyekuwa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Okaoni Septemba mwaka jana huko Dakau, Kibosho.

Akielezea tukio hilo, msichana huyo ambaye sasa amejifungua, alisema shangazi yake ambaye hana msaidizi nyumbani kwake, alimpigia simu bibi yake anayeishi naye, akimuomba yeye aende kumsaidia kufua nguo. 
Alipokwenda, kwanza aliambiwa atoe mbolea katika zizi la ng’ombe lakini akiwa huko, binamu yake, ambaye ni mtoto wa mama yake mkubwa, alimfuata na kutaka kumbaka, kabla ya kufanikiwa kukimbia.

Alisema alipomweleza shangazi yake kuhusu suala hilo, alimjibu kwa kilugha akimwambia kuwa asimwambie upuuzi, kitu ambacho kilimuuma binti huyo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15.

“Niliondoka baada ya shangazi kunijibu hivyo. Nikiwa nafua nguo, Agustin aliniita ndani, nikajua ananipa zingine ili nifue, lakini nilipoingia alinishika mkono na kunivutia chumbani kwake, akaniambia ole wangu nikipiga kelele au kumwambia mtu, atanifanyia kitu ambacho sitasahau, aliniziba mdomo, akanivua nguo na kuanza kuniingilia,” alisema binti huyo.

“Nilisikia maumivu makali sana, nikamwambia shangazi, lakini hakutaka kunisikiliza, nikamweleza pia yeye mwenyewe Agustin kuwa nimeumia sana, hakunijibu. Kesho yake aliniletea dawa nimeze, nikameza nikarudi kwa bibi yangu. Baada ya miezi 6 nikasikia tumbo linauma, nikajua nina minyoo nikamwambia shangazi akanipa dawa za minyoo, nikazimeza, hata hivyo sikuona dalili za kupona.

“Nikamwambia Agustin naumwa  tumbo, akaniambia nioge anipeleke hospitali, nilipima nikakutwa nina mimba ya miezi 5, alinichukua akanipeleka hospitali ya Mawezi, akaongea na daktari mmoja akampa dawa, sikujua ni za nini nilipotumia nilipatwa na kizunguzungu, kumbe zilikuwa ni za kutoa mimba, pia alinipeleka Arusha Mianzini kwenda kutoa mimba kwenye dispensari iliyoko huko, akapewa dawa anipe wakati tukiwa tumefika nyumbani.”

Baada ya zoezi hilo kushindikana, msichana  huyo alisema dada wa Agustin aitwaye Aniseta alimpigia simu rafiki yake mmoja aishiye Dar akimuomba aje Moshi kuna kazi anataka amsaidie.Inadaiwa kuwa rafiki huyo anayetajwa kwa jina moja la Najma alitumiwa nauli ya shilingi laki moja aende Moshi na alipofika, alimwambia kuwa kaka yake amempa mimba mtoto wa ndugu yake hivyo  wanataka wamtoroshe kumpeleka Dar akae mpaka ajifungue kwani kule polisi na walimu wanamfuatilia ili wamfunge.

Najma alipatikana na kukiri kwenda Moshi kumfuata binti huyo, lakini alipofika naye Dar, rafiki yake alipigia simu na kumtaka amdhuru binti huyo ili kupoteza ushahidi, jambo ambalo alilipinga licha ya wito wao wa mara kwa mara.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mloe, Salutary Mushi naye alisema ni kweli Agustin ana tabia ya kupenda kutoka na watoto wadogo, jambo ambalo limekuwa kero kubwa mtaani hapo kwani huyu si mtoto wa kwanza kumharibia maisha, akidai pia kuwahi kufanya hivyo kwa mtoto wa baba yake mkubwa.

Agustin mwenyewe hakupatikana licha ya kuwepo habari za kuachiwa kutoka kituo cha Polisi Moshi alikopelekwa kwa kosa hilo lililofunguliwa kwa faili namba MS/RB3336/014.
Powered by Blogger.